Monday, 11 September 2017

Kampuni ya madini yasitisha uchimbaji Tanzania


Kampuni ya uchimbaji almasi ya Petra Diamonds imesimamisha shughuli zake za uchimbaji katika mgodi wake uliopo Mwadui Shinyanga, Kaskazini Magharibi mwa Tanzania.
Hii imekuja siku chache tu baada ya kamati za bunge kuwasilisha ripoti zao kwa Rais John Magufuli kufuatia uchunguzi walioufanya katika sekta ya uchimbaji madini ya almasi na tanzanite.
Petra, ambao ndio wachimbaji wakubwa wa almasi nchini Tanzania, wamekuwa wamejikuta kuwa kampuni nyingine ya kigeni kuingia katika mgogoro serikali ya Tanzania katika harakati za kufanya mageuzi katika sekta ya uchimbaji madini nchini humo.
Wiki mbili zilizopita, mamlaka nchini Tanzania ziliripoti kukamatwa kwa vifurushi vya almasi katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere ambavyo vilikuwa ni mali ya Petra na vilikuwa mbioni kusafirishwa kwenda Ubelgiji kuuzwa.
Maafisa wa serikali walisema Petra ilidanganya juu ya kiasi na thamani ya almasi hizo ambapo, wakati kampuni ya Petra ikisema almasi hiyo ilikuwa na thamani ya dola za kimarekani milioni 14.8, uchunguzi wa serikali ulibaini almasi hiyo ilikuwa na thamani ya dola milioni 29.5.
Hata hivyo, Petra imekanusha tuhuma hizo na kusema kwanza wao ni wawazi katika kuripoti thamani ya almasi yake lakini pia ni wakala wa serikali ndio unaokisia na kutoa thamani ya almasi inayochimbwa na kampuni hiyo.
Mwandishi wetu Sammy Awami akiwa Dar es Salaam anasema katika waraka wake leo hii, Petra imesema pia kwamba baadhi ya maafisa wake wa ngazi za juu wanahojiwa na mamlaka nchini Tanzania kuhusiana na sakata hiyo.
Kuhusu kufungwa kwa mgodi wake wa Williamson uliopo Mwadui, Shinyanga, Petra imesema uamuzi huo wameufikia kutokana na sababu za "kiafya na kiusalama" na kwamba wanaendelea kutoa ushirikiano wao kwa serikali ya Tanzania katika uchunguzi wa mkasa unaoendelea hivi sasa.
Serikali ya Tanzania imeendelea na harakati zake za kimapinduzi katika sekta ya madini ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Rais Magufuli kuona sekta hiyo inachangia zaidi katika pato la taifa.
Tayari kuna sheria kali ambazo zimewekwa kuhakikisha kwamba sekta ya madini nchini Tanzania inabanwa katika kuchangia zaidi mapato kwa serikali.

No comments:

Post a Comment